Rais Jakaya Kikwete amewahakikishia viongozi wa waangalizi
wa kimataifa kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utafanyika kwa amani na
utulivu ikilinganishwa na zilizopita.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na viongozi hao Ikulu walikokwenda kujitambulisha.
Viongozi hao ni Rais mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan
anayeongoza ujumbe wa waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola na Rais
mstaafu wa Msumbiji, Armando Emilio Guebuza wa ujumbe wa Umoja wa Afrika
(AU).
“Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa amani na utulivu kuliko
miaka yote, kampeni zimeendeshwa kwa amani na utulivu. Nina imani kubwa
kabisa kuwa utakuwa huru na wa amani zaidi,” alisema
Jonathan alisema ujumbe wake una wataalamu waliobobea
kwenye siasa, uchaguzi, waandishi wa habari na vijana na una jukumu la
kufuatilia uchaguzi huo kabla, wakati na baada ya kupiga kesho.
Waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola wametoka Afrika Kusini, Botswana , India, Jamaica, Kenya, Malaysia na New Zealand.
Wengine wanatoka Papua New Guinea, Singapore, Sri Lanka,
Trinidad na Tobago, Uganda na Uingereza. Waangalizi kutoka AU wametoka
Afrika Kusini, Burundi, Botswana, Cameroon, Chad, Ethiopia, Gambia,
Ghana, Kenya, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Somalia, Sierra Leone,
Swaziland, Uganda, Shelisheli na Zambia. Waangalizi hao watasaidiwa na
Kamisheni ya Afrika, Bunge la Afrika na Taasisi ya Uchaguzi na
Demokrasia ya Afrika katika kazi yao hiyo.
Rais awaonya watumishi wa umma
Katika tukio jingine; Rais Kikwete amesema itakuwa vigumu
Tanzania kupiga hatua ya maendeleo ikiwa watumishi wa umma wataendeleza
ukiritimba kwenye sekta hiyo. Akizungumza juzi wakati na watumishi wa
umma katika hafla ya kumuaga, Rais aliyataja maeneo yanayotakiwa
kubadilisha mfumo katika kufanya uamuzi kuwa ni Mamlaka ya Udhibiti wa
Ununuzi wa Umma (PPRA), Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP), viongozi
wa wizara na sekta ya sheria.
Alisema kuna wawekezaji ambao walitaka kuwekeza nchini lakini kutokana na ukiritimba wamelazimika kwenda nchi nyingine.
“Tangu naingia madarakani miaka 10 iliyopita, nasikia
uwekezaji kwenye shamba la mifugo la Ruvu, mpaka naondoka uamuzi
haujafanyika wakati kampuni iliyotaka kuwekeza imeanza kazi Nigeria na
Gabone, sisi hatujafikia uamuzi,” alisema.
-
-

Comments
Post a Comment