Joseph Bulule ni mmoja kati ya wachimbaji watano waliokuwa
wamefukiwa na kifusi kwenye machimbo ya Nyangalata wilayani Kahama tangu
Oktoba 5, siku tatu baada ya Lowassa kurejesha fomu za kuwania urais
kwa tiketi ya Chadema.
Juhudi za kuwaokoa wachimbaji hao zilifanyika lakini
zikasitishwa baada ya muda kutokana na kutokuwapo na dalili za
mafanikio, kabla ya jitihada hizo kuanza tena baada ya wachimbaji
wengine kusikia sauti za wenzao wakiomba msaada kutoka chini ardhi.
Bulule, ambaye amelazwa Hospitali ya Halmashauri ya Kahama,
aliuliza swali hiyo mbele ya waandishi wa habari baada ya kupata
fahamu.
“Nani alishinda kwenye uchaguzi wa Rais,” aliuliza
waandishi akiwa amelala kitandani. “Lowassa alishinda? Maana sisi tangu
Oktoba 5, tulipofukiwa hatujui kinachoendelea. Uchaguzi umetukuta ndani
ya mashimo na hatujui matokeo ya uchaguzi.”
Uchaguzi wa Rais na wabunge ulifanyika siku ishirini
baadaye wakati juhudi za kuwaokoa zikiwa zimeshasitishwa. Katika matokeo
ya uchaguzi huo, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli
alishinda kwa kupata kura milioni 8.88, huku Lowassa, aliyekuwa anaungwa
mkono na vyama vinne, akishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni
6.07
Baada ya waandishi wa habari kumueleza kuwa aliyeshinda ni Dk Magufuli, mchimbaji madini huyo mdogo alionekana kukosa raha.
Kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Joseph
Ngowi jana mchana watu hao watano walianza kupatiwa chakula chepesi,
kama uji wenye maji mengi ambayo alisema yanasaidia utumbo kunyanyuka
baada ya kukaa siku 41 bila kupata chakula.
Alisema baada ya hatua hiyo wataanza kupewa chakula laini
na baada ya siku saba wataanzza kula chakula cha kawaida. Alisema wote
watano wapo kwenye usimamizi wa madaktari pamoja na wataalamu.
Wakiwa kwenye mgodi Oktoba 5, kifusi kilikatika na kufunika
mlango wa kutokea, hali iliyofanya waishi siku 41 kwa kunywa maji, kula
mende, vyura na magamba ya miti hadi walipookolewa Jumapili iliyopita
wakiwa hai.
c.mwananchi

Comments
Post a Comment