Ibara ya 51 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuhusu nafasi ya Waziri Mkuu inasema, “Kutakuwa na Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano atakayeteuliwa na Rais kwa kufuata masharti ya
ibara hii na ambaye kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Rais
kwa kiapo kinachohusika na kiti cha Waziri Mkuu kitakachowekwa na Bunge.
Kifungu cha (2) cha ibara hiyo kinasema, “Mapema
iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku kumi na nne, baada ya
kushika madaraka yake, Rais atamteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika
Jimbo la Uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi
zaidi bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi,
anayeelekea kuungwa mkono na wabunge waliowengi kuwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano, naye hatashika madaraka hayo mpaka kwanza uteuzi
wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na kura
za Wabunge walio wengi.”
Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti,
usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za
Serikali ya Jamhuri ya Muungano; atakuwa kiongozi wa shughuli za
Serikali bungeni, na kusimamia utekelezaji wa jambo lolote au mambo
yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe.
Kwa kuzingatia ibara hiyo, Rais John Magufuli anatarajiwa
kesho kuwasilisha bungeni jina la mbunge anayempendekeza awe Waziri Mkuu
wa Serikali ya Awamu ya Tano ili apitishwe na wabunge kabla ya
kuapishwa rasmi.
Tangu Dk Magufuli aingie madarakani watu wamekuwa
wakibashiri majina ya wabunge mbalimbali ambao wanaoonekana wanafaa
kuteuliwa kwa nafasi hiyo.
Hata katika viunga vya Bunge lililoanza kazi jana, wabunge
mbalimbali waliozungumza na Mwananchi kwa masharti ya kutotajwa gazetini
wameeleza kuwa bado suala hilo ni siri kubwa, hivyo hakuna haja ya
kujisumbua kulitafuta jina kwani wanasubiri hadi litajwe bungeni.
Mmoja wa wabunge hao alisema kuwa huenda waziri mkuu akatoka kati ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini au mikoa ya Kusini.
Mwingine alisema suala la nani atakuwa waziri mkuu ni la
kusubiri hadi Alhamisi Rais atakapoliwasilisha jina kwa kuwa hakuna mtu
anayelifahamu zaidi ya Rais na wasaidizi wake.
Hata hivyo baadhi ya wabunge walisema kuwa majina ambayo
yamekuwa yakitajwatajwa kuingia kwenye nafasi hiyo hayana nafasi kwa
kuwa Rais mwenyewe amekuwa msiri na mwenye msimamo.
Kwenye mitandao mbalimbali wamekuwa wakitajwa wabunge
wanaofikiriwa kushika nafasi hiyo kutokana na kanda wanazotoka mjadala
ambao utaisha kesho kwa kujua nani ni waziri mkuu.
Miongoni mwa wabunge wanaotabiriwa wanaweza kupata uteuzi
wa Dk Magufuli kuchukua nafasi hiyo ni Dk Harrison Mwakyembe (Kyela),
January Makamba (Bumbuli), William Lukuvi (Isimani), Profesa Sospeter
Muhongo (Musoma Vijijini) na Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi).
Makada hao wamekuwa wakitajwa kuwa wanaweza kuwa chaguo la
Rais Magufuli kwani mbali na kuwa na rekodi nzuri ya uchapakazi wana
sifa zinazowapa wigo mpana wa mmoja wao kuwa Waziri Mkuu atakayekuwa
msimamizi wa mkuu wa shughuli zake.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu
akizungumzia matarajio yake kwa waziri mkuu mpya alisema wao kama
wabunge wanahitaji mtu atakayeweza kusimamia shughuli za Serikali
bungeni na kusimamia utekelezaji wake. “Wabunge hawahitaji mtu picha
bali mtu anayefaa katika utendaji,” alisisitiza Lissu.
Mbali ya wabunge, watu mbalimbali wana shauku ya kufahamu
ni nani atakayepewa nafasi hiyo nyeti na kuitumikia kwa uadilifu, weledi
na juhudi kwa miaka mitano ijayo. Kama ilivyo ada, wengi wameendelea
kutabiri baadhi ya makada ambao wana sifa ya uchapakazi kama Dk
Magufuli, ambayo inakwenda sambamba na kauli mbiu ya Rais huyo wa
Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu.’
Inawawia vigumu wabunge kufahamu ni nani kati ya
walioshinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 25 atakayerithi mikoba ya
Mtoto wa Mkulima, Mizengo Pinda kwani Dk Magufuli siyo mtu wa kutabirika
katika uamuzi wake.

Comments
Post a Comment