Mapya yamezidi kuibuka katika sakata la upotevu wa
makontena 349 na ukwepaji kodi, baada ya Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA) kuwasimamisha kazi maofisa wake watatu kupisha uchunguzi.
Mbali na kusimamisha watumishi hao
wanaohusika na usimamizi
wa shughuli za Bandari kavu, TPA pia imepoteza mapato katika sakata
hilo lilisababisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupoteza Sh80
bilioni.
Hatua hiyo ya TPA kuwasimamisha watumishi wake imekuja mara
baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara ya kushtukiza
katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini upotevu wa mizigo hiyo.
Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Janeth Ruzangi
alisema jana katika mahojiano kuwa maofisa hao watatu walisimamishwa
Jumamosi ya wiki iliyopita, ikiwa ni siku moja baada ya ziara ya
Majaliwa.
“Kama sehemu ya uwajibikaji, tumewasimamisha ofisa mkuu wa kitengo kinachosimamia ICD na makarani wawili ili kupisha uchunguzi.
“Uchunguzi huo unaendelea ili kufahamu iwapo walihusika na
upotevu huo ama la au walijua au hawakufahamu suala hilo,” alisema
Ruzangi huku akikataa kuweka bayana majina ya watumishi hao.
Kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha muongozo wa gharama za
bandari wa mwaka 2013, mizigo yote ya ndani inayopitia bandarini hutozwa
asilimia 1.6 ya thamani ya mzigo iliyobainishwa na TRA wakati ile ya
nje hutozwa asilimia 1.25 katika tozo ijulikanayo kama “wharfage”.
Hata hivyo, katika makontena hayo 349 TPA ilipata mapato
yaliyohusu usimamizi pekee wa ushushaji wa mizigo hiyo huku ikipoteza
yale yanayotegemea tathmini ya TRA, ambayo kwa taarifa ya Waziri Mkuu
haikufanyika kiasi cha Serikali kupoteza Sh80 bilioni kama kodi.
Ruzangi alisema fedha zilizotajwa kupotea kama ukwepaji kodi katika upotevu wa makontena hayo, hazihusu mapato ya Bandari.
“Ni kweli hayo mapato ya awamu ya pili bila shaka na sisi
tuliyakosa,” alisema Ruzangi alipoulizwa kupoteza kiasi hicho cha fedha
ambacho alibainisha ni asimilia 1.6 ya Sh80 bilioni ambazo ni thamani
inayodai TRA.
Alisema Sh934.5 milioni zimepotea kama mapato ya bandari
katika sakata hilo linaloihusisha Kampuni ya Bandari Kavu ya Azam. Hata
hivyo, menejimenti ya Azam juzi ilikana kumiliki mali yoyote ya shehena
hiyo, zaidi ya kueleza kuwa makontena hayo yalikuwa ya wateja na kwamba
walikuwa wakitoa ushirikiano kufanikisha uchunguzi.
Ruzangi alisema makontena hayo 349 yaliingia kati ya Mei na
Oktoba mwaka huu na kwamba upotevu huo ni mkubwa kuwahi kutokea katika
historia ndani na nje ya bandari ukifuatiwa na upotevu wa makontena 21
ya vitenge mwaka 2012.
“Bandari yetu kwa sasa ni salama hakuna wizi tena kama
miaka ya nyuma. Kwa sasa tunafunga kamera za ulinzi 485 eneo lote la
bandari, kufunga wavu kwenye kuta na kuimarisha mfumo wa kielektroniki
wa ulinzi magetini,” alisema.
Ruzangi alisema mfumo wa Tehama wa TPA hauingiliani na ule
wa TRA uitwao Tancis, jambo ambalo baadhi ya wadau wanahisi ilitumika
njia ya kutumia udhaifu huo kukwepa mapato, lakini akaeleza mfumo
unaoingiliana utaanza kazi mwakani.
Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakala wa Shehana na Forodha,
(TAFFA), Edward Urio alisema katika sakata hilo, TRA ndiyo wanahusika
zaidi kutokana na kusimamia mchakato mzima wa uingizaji wa mzigo.
“Mali zote zinazoingia ni za TRA. Sitegemei bandari wawe na rekodi, halafu TRA wasiwe nazo,” alisema Urio.
“Kuna wasiwasi huenda rekodi za mzigo huo zilifutwa au
hazikuingizwa kabisa japo taarifa za mzigo huwafikia mapema kabisa
kutoka kwa kampuni ya meli inayosafirisha,” alisema.
Urio ambaye huusika na biashara ya uwakala wa shehena na
forodha, alisema Bandari Kavu zimekuwa zikiendesha biashara zao kwa
makandokando mengi yakiwemo kuongeza gharama zisizokuwa na mashiko.
Tayari watumishi tisa wa TRA wakiongozwa na Kamishna Mkuu
wa mamlaka hayo, Rished Bade wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa
sakata hilo la kwanza katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John
Magufuli.
By Nuzulack Dausen

Comments
Post a Comment