KAMATI ya Ulinzi na Usalama katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara,
imeteketeza ekari 56 za
mashamba ya bangi.
mashamba ya bangi.
Sambamba na hatua hiyo, pia kamati hiyo ikiongozwa na
Mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga, imekamata
magunia 20 ya dawa hizo za kulevya.
Kuteketezwa kwa mashamba na kukamatwa kwa bangi hiyo,
kumetokana na msako mkali wa kupamba na na kilimo cha zao hilo wilayani humu
uliofanyika kuanzia Februari 13, mwaka huu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema watu 14 wametiwa mbaroni na
wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo.
"Nimeunda kikosi kazi kikishirikiana na Kamati ya
Ulinzi na Usalama wilayani hapa cha kupambana, wakulima, wauzaji na
wasafirishaji wa dawa za kulevya ikiwamo mirungi kutoka nchi jirani ya
Kenya," alisema.
Luoga alisema msako huo wa siku tatu, ulifanyika katika
Kata za Mwema, Matongo na Kibasuka kwenye Vijiji vya Nyarwana, Matongo,
Korotambe, Nyamohonda, Wegita na Nyakunguru.
Alisema bado wanaendelea kuwasaka watu wengine
waliotoroka baada ya kuwatia mbaroni watuhumiwa 14 na kwamba kazi hiyo ni endelevu.
"Ninawaagiza viongozi wa vitongoji, vijiji,
watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa kwa vyombo vya
dola za watu wanaojihusisha na kilimo cha bangi, wauzaji wa dawa hizo za
kulevya na wasafirishaji wake ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya
sheria kiongozi yeyote atakayeshindwa kutoa taarifa hizo katika maeneo yake
atachukuliwa hatua za kinidhamu," alisema.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amewaonya wanaojihusisha na
kilimo, usafirishaji na uuzaji wa dawa hizo za kulevya, waache mara moja na
kuanzisha miradi mingine ikiwamo ya kilimo cha mazao ya chakula kama mahindi,
migomba, viazi vitamu, vitunguu, alizeti na mboga.
Wilaya ya Tarime ni moja ya wilaya zinazoongoza kwa mikoa
ya Kanda ya Ziwa katika kilimo cha bangi na soko kubwa la zao hilo liko nchi
jirani ya Kenya na husafirishwa kwenda Mwanza na kuuzwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Comments
Post a Comment