MWANAMKE mmoja raia wa Misri, anayeaminika
kuwa ndiye mwenye uzito mkubwa zaidi duniani, amewasili Mumbai , India ili kufanyiwa
upasuaji.
Eman Ahmed Abd El Aty mwenye umri wa miaka 36 ana uzani
wa kilo 500 ambaye anatakiwa
kufanyiwa upasuaji ili kumsaidia kupunguza uzito
wake.
Safari hiyo, ilikuwa ya kwanza kwake kuondoka nyumbani
katika kipindi cha miaka 25.
"Eman aliyesafiri kwa ndege ya EgyptAir aliwasili
katika uwanja wa ndege wa Mumbai majira ya saa kumi alfajiri na akafika
hospitalini Saifee mwendo wa saa kumi na mbili alfajiri. Kitanda maalum
alicholalia kiliinuliwa, akiwa kitandani kwa kutumia kreni," madaktari
walisema.
Alisafirishwa kwenda hospitalini kutoka uwanja wa ndege
kwa kutumia lori maalum lililofuatwa na gari la kuwabebea wagonjwa pamoja na
gari la polisi.
Katika hospitali ya Saifee, kuna chumba kilichojengwa
mahsusi kwa ajili yake.
Atakuwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa muda wa mwezi
mmoja kabla ya kufanyiwa upasuaji, madaktari wamesema.
Kwa sasa, atatunzwa na mtaalamu wa upasuaji Muffazal
Lakdawala na kundi lake la matabibu, ambao wamekuwa wakimtunza kwa karibu miezi
mitatu hata kufanikisha kusafirishwa kwake kutoka Misri.
Kutokana na ukweli kwamba hajatoka kitandani kwa miaka 25
iliyopita, alikuwa na hatari ya kuugua maradhi ya kupumua. Wakati akisafirishwa
na madaktari walichukua tahadhari kubwa na kumpa dawa za kuyeyusha damu
mwilini.
Kitanda alichosafirishwa nacho ni maalum kilichoundwa na
mafundi wa Misri kwa kuzingatia matakwa ya shirika la ndege la EgyptAir.
Kilikuwa na mitambo na vifaa vya huduma ya dharura.
Familia ya Eman Ahmed inasema alikuwa na uzani wa kilo
tano alipozaliwa kabla ya kupatikana na ugonjwa wa matende, ugonjwa ambao
unasababisha kufura kwa mwili kutokana na maambukizi ya vimelea.
Wakati alipofikisha umri wa miaka 11, uzani wake
uliongezeka maradufu na kuugua kiharusi ugonjwa uliomuacha kitandani kwa
kipindi kirefu cha maisha yake.
Daktari wa upasuaji wa kupunguza matumbo kwa lengo la
kutaka kupunguza uzani Muffazal Lakdawala hata hivyo aliambia BBC mwezi Desemba
kwamba anaamini Eman Ahmed haugui ugonjwa wa matende bali anaugua ugonjwa wa
kunenepa kupita kiasi ambao husababisha miguu kuvimba.
Ubalozi wa India mjini Cairo ulimkatalia kupewa visa bi
Abd El Aty kwa kuwa hakuweza kusafiri pekee.
Alipewa visa baada ya Dk. Lakdawala kutuma ujumbe katika
Twitter kwa waziri wa masuala ya kigeni nchini India Sushma Swaraj ambaye
alijibu kwa kutaka kutoa usaidizi.
Upasuaji wa kupunguza matumbo ili kupunguza uzani wa mtu
aliye na uzani mkubwa hutumika kama hatua ya mwisho ya kuwatibu watu walio na
uzani mkubwa na walio na mafuta mengi.

Comments
Post a Comment