Licha ya kusomea taaluma ya
ualimu katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Benjamin Ngowi hakukubali ajira aliyopewa
na Serikali badala yake
akaitumia falsafa inayopigiwa chapuo na kujiajiri.
Amefanya hivyo kwenye eneo ambalo
hakusomea bali kutokana na kipaji alichogundua kuwa nacho tangu akiwa mdogo.
Ingawa hakitoshi, anayo mipango ya kukuza kipato chake ili kufanikisha ndoto
alizonazo.
Benjamin ameamua kujiingiza
kwenye ujasiriamali wa kutengeneza viatu na anabainisha kwamba huwa anauza kwa
Sh25,000 kwa bei ya rejareja au Sh15,000 kwa bei ya jumla.
Anasema uwezo wake ni kutengeneza
kati ya jozi 50 mpaka 70 za viatu kwa wiki ambazo hazikidhi soko lake. Ili
kujiweka kwenye sehemu nzuri, amesajili kampuni yake ya Ngowi Production ambayo
anatarajia itakuwa na matawi kwenye mikoa yote nchini.
Wakati Serikali ikitekeleza
mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda, ipo hamasa ya kuwashawishi kuongeza
ubunifu na kujiajiri ili kukabiliana na uhaba wa ajira uliopo nchini kutokana
na kuongezeka kwa wahitimu kila mwaka.
Baada ya kuhitimu chuko kikuu
mwaka juzi, Benjamin alipangiwa kazi katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro
ambako hata hivyo hakwenda kuripoti licha ya kupata lawama nyingi kutoka kwa
mama yake.
Anasema kutokana na mtazamo wa watu
wengi kuamini zaidi kwenye kuajiriwa kuliko kujiajiri, mama yake pia
hakukubaliana naye alipokataa kwenda kufanyakazi aliyosomea.
“Wakati vituo vya kazi
vinatangazwa nilikuwa nimeshaanza kupata wateja wa kutosha hivyo ilikuwa vigumu
kuacha shughuli niliyokuwa nayo hasa kutoka mikoa ya kusini,” anasema Ngowi..
Anasema alitumia muda mwingi
kumshawishi mama yake aelewe anachokifanya kwani alikuwa anaamini katika
kuajiriwa kwake kuliko kujiajiri jambo lililompa wasiwasi kwa kuhisi shughuli
hiyo haitakuwa na faida na kuona mwanae anapoteza muda.
“Maneno ya watu ndiyo yalimpa
wasiwasi kwani baadhi yao walidiriki kunipigia simu na kunishawishi nikafanye
kazi niliyosomea,” anasema Ngowi.
Kutimiza malengo binafsi,
uvumilivu na ustahamilivu unahitajika ili kukabiliana na changamoto zilizopo
kabla ya kufikia mafanikio. Kutokana na haja ya kuboresha kipato, baadhi ya
watumishi huacha kazi na kujiajiri ili kukidhi mahitaji wakati wengine
wakiajiriwa na kujiajiri kwa wakati mmoja.
Benjamin, kijana mwenye umri wa
miaka 27, mkazi wa Tabata Relini jijini Dar es Salaam anatumia kipaji chake cha
kutengeneza viatu vya ngozi kabla hajamiliki kampuni ya ndoto yake na kuajiri
vijana wenzake kuwahudumia Watanzania kwa bidhaa zenye ubora.
Ujasiariamali
Ari ya kujiajiri na kuajiri
wengine ilimtia moyo na kumfanya aongeze juhudi ya kufanikisha adhima yake.
Anasema utengenezaji wa viatu hajafundishwa na mtu yoyote bali ni kipaji
kilichotokana na utundu wake akiwa mdogo.
“Nilikuwa na viatu nilivyovipenda
ambavyo vilikuwa vigumu hata ngozi yake ilipoisha ngozi iliendelea kubaki na
ilionekana bado mpya. Niliona naweza kufanya kitu, nilichukua begi langu
lililokuwa limechakaa na kutengeneza viatu vya wazi kwa kutumia soli hiyo,”
anasema Benjamin.
Baada ya kutengeneza kiatu cha
kwanza, aliendelea kufanya hivyo na akafanikiwa kuuza jozi moja kwa mwanafunzi
mwenzake jambo lililompa mwanga kuwa kuna fursa licha ya ugumu wa kupata soli
kwa ajili ya kutengeneza viatu vingi zaidi hivyo akawa anatengeneza
‘key-holder’ ndogo na kuwauzia wanafunzi wenzake.
Akiwa kidato cha tano, aliendelea
kutengeneza viatu na kuwauzia wanafunzi wenzake. “Kutokana na kukosa mtaji wa
kununua ngozi, nilikuwa natengeneza kwa kutumia mabegi chakavu yaliyokuwa
yakiuzwa kwa bei rahisi katika Soko la Karume,” anasema.
Kwa sasa anatengeneza kati ya
jozi 50 mpaka 70 kwa wiki na wateja wake wakubwa wa jumla wanatoka mikoa ya
Lindi, Mtwara na Tabora.
Anasema mkakati wake ni
kuimarisha ubora wa bidhaa zake ili kuwapa wateja wake kitu chenye thamani na
kuongeza ushindani sokoni ambako kuna wazalishaji wengi kutoka ndani na nje ya
nchi.
Ili kukabiliana na ushindani
uliopo, anasema anapenda kujifunza kila aina mpya ya viatu inayoingia sokoni au
mtandaoni kwa nia ya kukidhi ubora wanaotaka wateja wake.
Kama anayojifunza kupitia
mitandao mbalimbali ya kijamii, anasema huitumia kutafuta wateja pia hasa
kurasa zake za Facebook na Instagram.
Mpaka sasa ameajiri vijana
wenzake wawili anaoshirikiana nao kwenye shughuli hiyo. Mmoja kati yao,
Goodluck Lyamuya ambaye ni mhitimu wa stashahada ya masuala ya umeme anasema
alihamasika baada ya kuona mwenzake amejiajiri na kuamua kuungana naye.
“Najivunia kufanya naye kazi
kwani anapenda kuona vijana wenzake wakijishughulisha badala ya kukaa vijiweni
bila kazi ya kufanya,” anasema Goodluck.
Mafanikio
Kutokana na shughuli yake,
ameweza kubadilisha mazingira ya nyumbani kwao kwa kuweka umeme na kuboresha
kilimo. Ana maduka mawili anayoyatumia kuuza na kusambaza bidhaa
anazotengeneza.
Ili kuboresha bidhaa zake,
amefanikiwa kununua cherehani ya kushonea viatu, mashine ya kupiga msasa soli
na ya kulinganisha kuta za viatu. Haya yote ameyafanya kutokana na mtaji wa
Sh300,000 alioanza nao.
Katika mipango yake ya muda
mrefu, ana ndoto ya kufungua duka katika kila mkoa ili kuwafikia wateja wake na
kuwavalisha Watanzania viatu vinavyotengenezwa ndani ya nchi badala ya vile
vilivyotumika nje (mitumba).
Changamoto
Kutokana na kusomea masuala ya
elimu, anasema alikuwa hana ujuzi wa ujasiriamali jambo lilimpa wakati wa
kusajili wa biashara hivyo kulazimika kujifunza taratibu kadri siku zilivyozidi
kwenda.
Upatikanaji wa malighafi ulikuwa
ni jambo gumu kwani awali alikuwa anashindwa kutambua aina tofauti za ngozi na
kuchukua ngozi duni na viatu alivyotengeneza vilionekana kukosa ubora.
Kutokana na kutokuwa na mafunzo
na vifaa maalumu amekuwa akipoteza malighafi pindi alipokuwa anahitaji
kutengeneza aina mpya ya viatu aliyoiona hivyo jozi ya kwanza ilikuwa ya
majaribio kabla hajakamilisha aliyokuwa akiitaka.
Zana za uzalishaji zinauzwa ghali
na kuwashinda wajasiriamali wadogo kutengeneza bidhaa bora zitakazoshindana na
za nje,” anasema.
Licha ya wajasiriamali, mamlaka
kadhaa za Serikali zinaiona fursa iliyopo kwenye sekta ya ngozi hivyo
kujitokeza na kuiendeleza. Mapema mwaka huu, Mamalaka ya Maendeleo ya Biashara
(Tantrade) kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT)
iliendesha semina ya kuwajengea uwezo wafugaji na wachinjaji wa kusindika ngozi
za mifugo yao.
Semina hiyo pia ilikusudia kuwapa ujuzi wa kuziona na kuzitumia fursa
zilizopo kwenye ngozi na bidhaa zake kwa kuwaelimisha wafugaji, wasafirishaji,
wachinjaji na wasindikaji ili kuongeza thamani ya mazao hayo nchini

Comments
Post a Comment