Ujio wa Katibu UN, Rais amepoteza fursa kimataifa!
Nimesikitishwa na kushangazwa sana na
hatua ya Mhe Rais,
John Magufuli, kutofanya mazungumzo ya ana kwa ana na Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Gutteres, aliyepita nchini jana akitokea
Ethiopia na Kenya, alikofanya mazungumzo na viongozi wakuu wa nchi hizo.
Hatua ya Rais kumtuma Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Balozi Agustino Mahige, kuzungumza na Katibu wa UN
huku Rais mwenyewe akiwa yupo nchini, haikuwa sawa kiitifaki wala
kimkakati.
Hatua hiyo imezidi kupunguza ushawishi wa Tanzania kwenye
jumuiya ya kimataifa kwa kushindwa kuzitumia vizuri fursa za kimataifa
zinazojitokeza katika kufanikisha utekelezaji wa sera ya diplomasia ya
uchumi na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030.
Ujio wa Katibu huyu mpya wa UN aliyeingia madarakani tarehe
1 Januari mwaka huu, ulikuwa ni fursa kubwa na ya kipekee sana kwa
Rais, ambaye ndiye Mwanadiplomasia namba moja, kufanya mazungumzo na
kupenyeza si tu maslahi na ushauri wa Tanzania kwa UN, bali pia
kupenyeza changamoto na maslahi mapana ya jumuiya nzima ya Afrika ya
Mashariki ambayo Rais ndiye Mwenyekiti wake. Ni jambo la aibu kwa Rais
kuukimbia wajibu wake huu muhimu kwa nchi!
Wakati Rais Kenyata wa Kenya alivunja ratiba zake zote na
kuona ulazima wa kufanya mazungumzo na Katibu wa UN; na wakazungumza juu
ya kushughulikia matatizo ya njaa, ukame, ugaidi na changamoto za hali
mbaya ya usalama hasa kwa nchi jirani za Somalia, Burundi na Sudani;
Mwenyekiti Magufuli anayeongoza Jumuiya nzima ya Afrika ya Mashariki,
alichagua kwenda 'kujificha' Dodoma! Huu ni ushahidi wa wazi wa Rais
kukosa ajenda na kushindwa kuona fursa.
Ikumbukwe kuwa matatizo ya ukame na njaa ambayo Rais
Kenyata aliyazungumza na Katibu wa UN, ni sehemu ya matatizo makubwa
yanayoisibu Tanzania pia hivi sasa. Matatizo haya pia yams kwenye
Malengo ya Maendeleo Endelevu yaliyopitishwa na wakuu wa nchi wanachama
wa UN ikiwemo Tanzania. Kwa mujibu wa Malengo hayo, wajibu wa UN, pamoja
na mambo mengine, ni kuhamasisha jumuiya ya kimataifa hasa nchi tajiri
kuwekeza mikakati na raslimali za kutosha ili kukabiliana na mabadiliko
ya tabia ya nchi (climate change), kusaidia mikakati ya kuboresha kilimo
na kukabiliana na njaa hususani kwa nchi zilizo kusini mwa jangwa la
Sahara ikiwemo Tanzania. Wakati Wilaya mbalimbali nchini zikiwa kwenye
baa la njaa na ukame, inasikitisha kwa Kiongozi Mkuu wa nchi kushindwa
kuona fursa na ulazima wa kuyazungumza kwa uzito masuala haya na
Kiongozi huyu wa UN!
Wakati serikali ya Rais Magufuli ikidai inapambana na
madawa ya kulevya na wakati madawa hayo yakiwa yanaingizwa nchini kutoka
nchi mbalimbali duniani; nilitarajia kumuona Mkuu wetu wa nchi
akikutana na Katibu wa UN na kujadili suala hili. Alipaswa kuishawishi
UN kuchukua hatua madhubuti ya kuzibana na kudhibiti uzalishaji wa
madawa ya kulevya kwani kushamiri kwa biashara hiyo kunahatarisha pia
amani na maendeleo ya watu hasa vijana duniani kote. Jitihada za
kupambana na madawa ya kulevya hapa nchini zitakuwa ni za "kutwanga maji
kwenye kinu" kama hazitaishirikisha vizuri jumuiya ya kimataifa. Ni
ajabu kuwa Rais hakuiona fursa adhimu ya kukutana na Katibu wa UN ili
kutanua vita dhidi ya madawa ya kulevya kwa kuvitafutia msukumo wa
kimataifa.
Kwa uzito wa majukumu yake na ushawishi wa nafasi yake kwa
kimataifa, Katibu wa UN ni Kiongozi mwenye hadhi na umuhimu mkubwa sana
Duniani. Kwa kawaida huyu ndiye msemaji na muwasilishaji mkuu wa maslahi
ya nchi wanachama katika mikutano mikuu ya UN na kwenye vikao vya
mabaraza yake likiwemo Baraza la Ulinzi na Usalama na Baraza
linalohusika na Maendeleo ya Uchumi na Jamii (Economic and Social
Council). Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN Charter) pamoja na majukumu
mengine, umempa Katibu UN, fursa ya kuwasilisha jambo lolote kwenye
vikao hivyo, ambalo kwa mtazamo wake, linaweza kusaidia katika kudumisha
amani na usalama` na` ustawi wa nchi wanachama. Kwa namna yoyote ile,
Kiongozi mwenye hadhi na umuhimu mkubwa hivi duniani, alipofunga safari
kuitembelea Tanzania, hata kama ni kwa mazungumzo ya dakika chache,
haikupaswa apokelewe na kuzungumza na Waziri pekee. Hadhi inayolingana
na Kiongozi mwenye dhima ya kidunia, ni Rais wa nchi.
Haikuwa sawa hata kidogo kwa Rais kumkwepa Katibu wa UN na
kukimbilia Dodoma kwa kisingizio cha majukumu ya chama, ilihali
alishajua mapema juu ya ujio wa Kiongozi huyo;. Na kulikuwa uwezekano wa
Rais kutoka Dodoma na kufanya mazungumzo mafupi na Kiongozi huyo na
kurudi kwenye majukumu yake ya kawaida, lakini ha kufanya hivyo. Kwanini
vikao vya CCM viwe muhimu zaidi kwake kuliko maslahi ya Watanzania
wote?
Kwa mara nyingine tena, namtaka Mhe Rais kuyapa umuhimu na
ulazima wa kutosha masuala ya kimataifa. Tanzania si kisiwa...hata
akusanye kodi nyingi kiasi gani, hata atumbue majipu mengin kiasi gani,
bado Tanzania haitaweza kupata maendeleo ya haraka kama Rais atapuuza
ushirikiano wa kimataifa.
Ninaamini hatua ya Rais Magufuli kutokupata msukumo ndani
ya nafsi yake wa kukutana na Katibu wa UN, kunatokana na kutokuwa na
ajenda yoyote iliyobayana ya kimataifa anayoisimamia. Ni dhahiri kuwa
Ikulu ni kitu gani Tanzania inakitafuta au inakisimamia kwenye Jumuiya
ya kimataifa. Wangekuwa na ajenda, Rais asingeiacha fursa hiyo ipite
hivi hivi.
Kwa mara nyingine tena, namshauri Mhe Rais awatumie vizuri
wataalam na wasomi wa nchi hii ili wamwongoze vizuri zaidi jinsi ya
kuongoza nchi. Wamsaidie kuipata ajenda ya Tanzania kimataifa na
wamshauri jinsi ya kuzitumia vizuri fursa adhimu za kidiplomasia
zinazojitokeza kushawishi na` kusukuma maslahi ya nchi kimataifa. Asione
tabu kuutekeleza ushauri wangu. Tanzania ni yetu sote!
Imetolewa leo tarehe 11 March, 2017
Peter Simon Msigwa
Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda.
Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda.

Comments
Post a Comment