JESHI la Polisi mkoani Dodoma
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania
(TFDA), limekamatwa shehena ya pombe kali zilizofungashwa katika mifuko ya
plastiki, maarufu kama viroba, zenye uzito wa
tani 50.57.
Pombe hizo zenye thamani ya Sh. milioni 354.4 zimekamatwa
zimehifadhiwa kwenye makasha 3,972 ndani ya ghala la wafanyabiashara wawili
wanaomiliki kampuni ya Takawedo Investment iliyoko Kisasa, manispaa ya Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, aliwataja
wafanyabiashara waliokamatwa wakimiliki shehena hiyo ni Alexander Lipindo na
ndugu yake William Lupindo.
Mambosasa alitaja aina ya pombe zilizokamatwa kwa
wafanyabiashara hao ni konyagi katoni 1,399, Valeur katoni 712, Kiroba Original
1,782, Bismark katoni 24 na katoni 55 za Zanzi.
Alisema mpaka sasa shehena hiyo imezuiwa katika ghala hilo na kuwekewa utepe
maalum wa TFDA ili isiondolewe sehemu hiyo.
Kamanda huyo alisema kutokana na kukamatwa kwa shehena
hiyo, wamiliki hao hawataruhusiwa kusambaza mitaani hadi maelekezo mengine ya
serikali yatakapotolewa.
"Ninawaomba
wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua wasambazaji na
watumiaji wa pombe hizi kali zilizopigwa marufuku na serikali,” alisema
Mambosasa.

Comments
Post a Comment