MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu
na Majini (Sumatra) Mkoa wa Arusha
inapanga kuondoa usafiri wa magari madogo ya
abiria jijini Arusha maarufu vifodi kwa kuwa hauendani na hadhi ya jiji.
Akizungumza mjini hapa juzi, Meneja wa Sumatra mkoani
hapa, Allen Mwani, alisema mamlaka hiyo kwa sasa ipo katika upembuzi yakinifu
wa kuondoa usafiri wa vifodi kutokana na kutokuwa na viwango vinavyotakiwa
kusafirisha abiria.
Alisema mamlaka hiyo inahamasisha wadau kuungana na
kuleta mabasi makubwa ya usafirishaji abiria (City Bus) katika jiji la Arusha
ili kuendana na hadhi ya jiji hilo.
Mwani alisema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa
Halmashauri ya Jiji la Arusha juzi.
"Usafiri wa abiria mjini kwa kutumia vifodi umepitwa
na wakati na sasa tuna mpango wa kuingiza usafirishaji wa mabasi makubwa (City
Bus)," alisema.
Katika kikao hicho, pia Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Majitaka na Majisafi Mkoa wa Arusha (AUWSA), Ruth Koya, alieleza changamoto
kubwa inayowakabili wananchi kwa sasa ya uhaba wa maji.
Alisema wanategemea kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa
maji utakaotoa lita milioni 200 wakati mahitaji ni lita milioni 94 tofauti.
Alisema kwa sasa kiwango cha maji kinachozalishwa ni lita milioni 35 tu ambacho
hakitoshelezi hata nusu ya mahitaji ya wananchi.
Kwa upande wake, Shirika la Umeme mkoani hapa lilitoa
ufafanuzi kuhusu kukatikakatika kwa huduma ya umeme, likisema kunatokana na
maboresho yanayofanywa.
Ufafanuzi huo ulitolewa na Mhandishi wa Mipango na
Ubunifu wa shirika hilo, Beatus Rwegoshora.
“Tanesco iko katika maboresho ya huduma kwa wateja na
hivyo tatizo hilo litapungua na pia shirika lipo katika mpango mahususi wa
kuwawezesha wananchi kupata taarifa zote za msingi kupitia simu za kiganjani,”
alisema.

Comments
Post a Comment