Tunaposherehekea
Sikukuu ya Pasaka, tunapokumbuka kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo wa Nazareti,
ni
muhimu kutafakari juu ya matukio haya ambayo kumbukukumbu yake imedumu hapa
duniani zaidi ya miaka elfu mbili sasa.
Kila
mwaka tunayakumbuka matukio haya, ni yale yale. Ni kufa na kufufuka, kiasi
kwamba wakati mwingine maana inapotea na watu wanabaki kutekeleza tu kama mazoea. Ili matukio
haya yawe na maana katika maisha yetu, kuna umuhimu wa kuanza utamaduni wa
kutafakari. Tujiulize maswali. Je, wakati huu wa Pasaka, makaburi yanazungumza
na watu wanafufuka?
Je,
kuna ufufuko katika nyakati hizi tulizomo? Au ufufuko ulikuwa ni wa Yesu Kristo
peke yake? Miaka ya nyuma, mimi binafsi wakati wa kipindi kama
hiki cha Pasaka, nilipokea ujumbe kutoka makaburini (usiwe na mawazo ya
makaburi ya Kinondoni na madhambi yanayoendelea kwenye makaburi hayo). Ujumbe
huu ni kitu kilichonifikia kwa wakati wake. Ni ufufuko wa aina yake. Bahati
mbaya ni ufufuko unaotokea nyakati za ubishi na maendeleo makubwa ya sayansi na
teknolojia. Ni ufufuko ambao bila kushuhudiwa na Wazungu tutasema ni porojo.
Ufufuko
halikuwa jambo geni katika maisha na utamaduni wa Mwafrika, falsafa na teolojia
iliyokuwa imeuzunguka ufufuko wa Mwafrika ni kati ya mambo mazuri ya utamaduni
wa Mwafrika yaliyofutwa na Wazungu wakati wakileta ukoloni,ustaarabu na dini
zao hapa kwetu.
Mwafrika
akikutwa na mifupa ya wafu, unakuwa ushirikina, Mzungu akikutwa na mifupa ya
wafu, inakuwa ni masalia ya watakatifu na mifupa hiyo inatunzwa kila sehemu,
makanisani, majumbani na kwenye pete za watu wakubwa katika jamii kama vile maaskofu.
Mwafrika
akiabudu chini ya mti, akajenga vibanda vya kuabudu, akautukuza mti na kuuona kama mwakilishi wa Mungu aliye hai katika jamii, inaitwa
kuiabudu miungu na upagani. Mzungu, akiabudu kwenye sanamu ya Bikira Maria na
watakatifu wengine, hiyo ni imani iliyo sahihi. Si lengo langu kupiga porojo na
wala si tabia yangu kuwatania wasomaji wangu.Nimekuwa nikijitahidi kuwaletea
wasomaji wangu mada zenye ukweli, zenye kuelimisha, kuburudisha na kuchokoza
mawazo. Sijaenda nje ya malengo yangu.
Kisa
hiki ninachokisimulia leo hii ni cha kweli.
Mwaka
wa 2005, wakati ninatafakari kuhusu ujumbe wa Pasaka, nilipata barua pepe
kutoka kwa kijana aliyekuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Si kati ya barua zinazoingia
bila ya anwani ingawa kwa makusudi nimeamua kufuta anwani na jina la kijana
huyo. Hata hivyo sifa za mtu na mahali anapoishi vinamtangaza kuliko jina lake.
Mfano akina John ni wangapi? Akina Mutembei ni wangapi? Akina Masanja ni
wangapi? Akina Nassor ni wangapi? La msingi si jina, ni huyo mwenye jina
kafanya nini katika jamii, mchango wake ni upi? Anachangia kukua kwa haki, wema
na huruma katika jamii au anachangia kuzalisha dhuruma, ukatili na unyanyasaji?
Ni
kama kijana huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
aliyasoma mawazo yangu, labda alitumia teknolojia ya Mwafrika, teknolojia
isiyoendelezwa kama ile ya kuruka na kupaa juu
ya ungo, alijua jinsi nilivyokuwa na wakati mgumu, wa kuandaa ujumbe wa Pasaka.
Labda wewe hupati shida, inawezekana Pasaka kwako ni kitu cha kawaida,
Mungu-tunafundishwa ana nafsi tatu, Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho
Mtakatifu, wote ni Mungu mmoja-Muumba Mbingu na dunia, Mungu anayeumba viumbe
vyote, akamatwe, apigwe na kuuawa na binadamu. Mungu afe! Kinyume na mafundisho
kwamba yeye yupo jana, leo na kesho, yeye hana mwanzo wala mwisho, yeye ni Alfa
na Omega. Anakufa wakati wa Pasaka! Lakini kwa kuonyesha umungu wake,(kana
kwamba anapima nguvu zake na Mungu mwingine) afufuke siku ya tatu. Akifufuka,
ajionyeshe kwa wanawake, lakini ukweli huu uenezwe na wanaume, madaraka yote
kuuzunguka ukweli huu ulioshuhudiwa na wanawake, utawaliwe na wanaume! Maana
viongozi wa dini za kikristo na hasa Kanisa Katoliki ni wanaume watupu.
Mungu
au Mwana wa Mungu, kama tunavyofundishwa ni
kwamba alikufa kufuta dhambi. Sasa ni miaka elfu mbili baada ya kufa na
kufufuka kwake, dhambi bado ina utawala ulimwengu wetu. Uonevu, dhuruma na
ukiukwaji wa haki za binadamu ni maua
yaliyoupamba ulimwengu wetu. Tunawashuhudia wenye nguvu hata na wale
wanaoongozwa na “In God we Trust” wanaendelea kutoa uhai wa watu wasiokuwa na
hatia. Yesu, aliyeishinda dhambi kwa kifo na ufufuko wake, anatumiwa kuendeleza
dhambi na kuieneza duniani kote. Tunashuhudia wenye mali wanaendelea kuneemeka zaidi
wakati masikini wanaendelea kunyong’onyea. Chuki, hasira, visasi, ubaguzi wa
rangi na jinsia ni vitu vinavyoutawala ulimwengu wetu katika nyanja zote, iwe
ni serikali au dini. Ubinadamu unaendelea kuogelea katika dimbwi la dhambi kubwa
kiasi kwamba na huyo Yesu anayetajwa kuzifuta dhambi alifanya kazi bure.
Nilikuwa katika tafakari hii ndipo barua pepe ya kichwa cha habari: Ujumbe
Kutoka Makaburini, ikaingia. Nimeinukuu yote jinsi ilivyo. Uisome, ili
tutafakari sote:
“Mpendwa
Karugendo, shikamoo.Mwezi Januari nilibahatika kutembelea eneo la Mazimbu
Morogoro yalipo makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini.Hakika baada ya
kutoka huko naona sina raha maishani mwangu.Hata hivyo nimeonelea
nikushirikishe sauti hii niliyoisikia hata kama
huenda ulishawahi kufika na kushuhudia mwenyewe nakuhakikishia mwangwi wake
umebadilika.
“Baada
ya kufika makaburini ambayo yanatunzwa vema kuliko ya ndugu zetu wanaozikwa
Kinondoni au Mburahati, niliona kibao chenye ujumbe ambao umeweka alama katika
maisha yangu. Maneno haya yalisomeka hivi:
“Ours
was not for glory nor personal distinction but it was due for the noble cause
of our time and the liberation of humanity of the entire community of South Africa”.
“Wakati
bado nimepigwa ganzi na ujumbe huo huku nisijue la kufanya, wenzangu niliokuwa
nao yapata kama ishirini hivi wao walikuwa
wanashughulika na kupiga picha za ukumbusho. Nilidhani labda mimi ni mjinga
kushughulika na kisicho na maana badala ya kuweka kumbukumbu ili nije
nikawaonyeshe watu kwamba nani nilishawahi kutembelea hapo.
“Hata
hivyo nilihitimisha kuwa mtu mwenye akili hawezi kushughulika na mambo mengine
na kuacha ujumbe wa kutisha, wa kijasiri wa kizalendo, wa kujitoa mhanga kama huo. Basi nilijua ndio elimu yetu ya siku hizi maana
imekaa kiutandawazi.
“Kumbe
vifo vyao havikuwa ili waandikwe kwenye majina ya vitabu vya historia na
kuimbwa kwenye nyimbo huku wakisifiwa kila mara! Kumbe kufungwa kwa Mandela
hakukuwa kukuza jina la ukoo. Bila shaka walijua wazi kuwa wanachokipigania
wanaweza wasikifaidi lakini kwa utu wao na vizazi vijavyo walilala mistuni kama wanyama.
“Swali
lilinijia kuwa, Je, ukombozi wa utu wa mwanadamu sasa umekwisha? Uliondoka na
kwisha kwa ubaguzi? La hasha! bado tu watumwa wa wageni na hata ndugu
zetu.Ndipo nikaenda mbali kuwa watu wanalala darasani ili wapate madgrii wawe
maprofesa kwa ajili ya kukomboa wenzao au kukuza jina tu.Na rais na wabunge
wanataka nafasi hiyo kama ujumbe wa makaburi ulivyo au ni “for glory and
personal distinction”.
Wasalaam
.”
Tukiacha
maswali mengine yasiyokuwa na majibu au yale yaliyo juu ya akili zetu,
tunaambiwa kwamba Yesu, alikufa ili kuwakomboa wanadamu. Hakufa ili apate
heshima au jina lake
litukuzwe. Aliwafia
wengine. Alijitoa muhanga. Alikufa ili kwa kifo chake wengine wapate uhai tele.
Ndo
maana, ujumbe wa kijana huyu ulinigusa sana.
Maandishi aliyoyasoma kwenye makaburi hayo ni ya kutufikirisha sisi sote
tunaosherehekea kifo na ufufuko wa Bwana Yesu. Wafuasi ni wengi na madhehebu ni
mengi pia. Kila mtu anajitahidi kumtangaza Yesu aliyekufa na kufufuka. Je
tunakufa na kufufuka na huyo Kristo? Je tunawafia wengine, tunalifia taifa letu
la Tanzania?
Imani hii ya kufa na kufufuka inasaidia kuujenga uzalendo miongoni mwetu? Ili makaburi yatoe ujumbe, ni lazima waliozikwa kwenye
makaburi hayo wafufuke. Ufufuko kama ule alioushuhudia kijana wetu wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam,
pale Morogoro. Ukweli kwamba makaburi ya Morogoro ya wapiganaji wa Afrika
Kusini yaliweza kuugusa moyo wa kijana huyu aliyeyatembelea.
Maneno
hayo yaliyoandikwa juu ya makaburi ya Morogoro, yanaonyesha kwamba makaburi
hayo yako wazi na waliozikwa kwenye makaburi hayo wamefufuka! Ni sawa na ujumbe
ule tunaoupata siku ya Pasaka. Wanawake, waliokwenda kaburini walimkuta
malaika, akawambia Yesu, amefufuka na kaburi liko wazi. Wakati wale walioandika
Injili wanatusimulia juu ya malaika kwenye kaburi, huyu kijana wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam,
anatuelezea maandishi aliyoyasoma kwenye makaburi yakamwingia rohoni mwake hadi
anathubutu kusema hivi: “Swali lilinijia kuwa Je ukombozi wa utu wa mwanadamu
sasa umekwisha? Uliondoka na kwisha kwa ubaguzi? La hasha! bado tu watumwa wa
wageni na hata ndugu zetu.Ndipo nikaenda mbali kuwa watu wanalala darasani ili
wapate madgrii wawe maprofesa kwa ajili ya kukomboa wenzao au kukuza jina tu.Na
rais na wabunge wanataka nafasi hiyo kama ujumbe wa makaburi ulivyo au ni “for
glory and personal distinction”. Kwa maneno mengine maandishi kwenye makaburi
ya Morogoro ni sawa na Malaika aliyekutwa kwenye kaburi la Yesu, ni ujumbe
unaoelezea yale tusiyoweza kuyaelewa kwa akili zetu za kawaida.
Pasaka
inaweza kuwa na maana kwetu sisi tunaomwamini Kristo na wale wote
waliotuzunguka, tukimfuata yeye. Tukiyatoa maisha yetu kwa ndugu zetu,
tukikubali kufa na kufufuka, tukijiweka kwenye hali ya kuyaacha makaburi yetu
yakazungumza nyuma yetu.
Ni
sherehe kama nyingine, ndiyo tule tunywe na
kufurahi. Ni sherehe kama nyingine tuvae nguo
na kupendeza. Lakini tusiishie hapo, twende zaidi, tutafakari na kujiuliza
maswali mengi yenye majibu na yasiyokuwa na majibu. Kila Mtanzania
aliyebahatika kuisherehekea Pasaka, ya mwaka huu, ajiulize kama
kweli inamsaidia kumpenda jirani yake, inamsaidia kulipenda taifa. Je anaweza
kuyatoa maisha yake kwa wengine?
Ujumbe
tunaoupata ni kwamba anayetoa maisha yake kwa wengine, anayetoa maisha yake kwa
taifa lake, hafi, anaishi milele. Hata akifa anafufuka. Huu ndiyo ujumbe wa
Pasaka. Ni ujumbe wa kumgusa kila mtu aliye Mkristo na asiyekuwa Mkristo. Ni
ujumbe wa familia nzima ya Kitanzania.
Kitu
kilicho muhimu wakati huu, kitu ambacho ni lazima kimguse kila Mtanzania ni
kuujenga uzalendo wa taifa letu. Kila mtu kwa nafasi yake. Sherehe zote za dini
zetu zilenge katika kuujenga uzalendo wa taifa letu. Iwe ni Sikukuu ya Iddi,
Krisimas, Pasaka, Mavuno,Jando na Unyago zote zilenge katika kuujenga uzalendo
wa taifa letu.
Ninawatakia
Pasaka njema yenye mwanga mpya. Ufufuko utuletee uhai, matumaini, mshikamano na
uzalendo uliotukuka kama ule wa wapigania
uhuru wa Afrika Kusini.
Mwandishi Padri Privatus
Karugendo

Comments
Post a Comment