Zaidi ya Wafanyakazi 400 wa Serikali wanatarajia
kuondolewa kazini mkoani Morogoro kutokana na kushindwa kujiendeleza
kielimu baada ya kuajiriwa miaka 13 iliyopita wakiwa na vyeti vya elimu
ya msingi.
Watumishi hao ambao wengi wao ni wauguzi, wahudumu wa
afya, madereva, wahudumu wa ofisi, watendaji wa mitaa, vijiji na kata
tayari wamenyimwa mishahara yao ya mwezi huu.
Akizungumzia zoezi hilo aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya
Kimamba wilayani Kilosa, Mashaka Motile amesema katika wilaya hiyo
watumishi zaidi ya 80 wamenyimwa mshahara bila maelezo yoyote na
walipofuatilia ndipo walipofahamishwa kuwa walipewa muda wa kujiendeleza
na wameshindwa kufanya hivyo.
“Hakuna barua yoyote tuliyopewa ya kusimamishwa kazi
ila mshahara wa Julai hatujapewa na tulipofuatilia tuliambiwa kuna
waraka wa Serikali unaosema wale wote walioajiriwa kuanzia mwezi Mei 20,
2004 wakiwa na elimu ya msingi na wameshindwa kujiendeleza wanatakiwa
kuondolewa,” amesema.
Motile anasema yeye na baadhi ya watendaji wengine
walisimamishwa kazi kimakosa kwani agizo linasema wasimamishwe kazi
walioajiriwa kuanzia Mei 20, 2004 lakini wao waliajiriwa Mei Mosi, 2004.
Akizungumzia uamuzi huo wa Serikali, mhudumu wa afya
wa manispaa ya Morogoro ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema uamuzi
huo umekuwa wa ghafla mno na haujatoa muda wa wao kujiendeleza.
“Naiomba serikali ituongeze japo miaka mitatu ili
tuweze kujiendeleza maana hivi tulivyosimamishwa kazi ghafla familia
zetu zitaathirika sana na kuna hatari ya watoto wetu kuacha shule,
tunaomba tuongezewe muda,” amesema.
Alipotakiwa kuzungumzia zoezi hilo Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya Kilosa, Kessy Mkambala alisema bado zoezi
linaendelea litakapokamilika ndo ataweza kulizungumzia.
Naye Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za
Mitaa (TALGWU) mkoani Morogoro, Lawrence Mdega amesema wamepokea
malalamiko toka kwa wafanyakazi zaidi ya 150 wanaolalamika kuondolewa
kwa kuwa wana elimu ya msingi.
“Nimeshawasilisha haya malalamiko makao makuu ya
TALGWU ili washughulikie lakini tunachotaka watumishi hawa walipwe
mshahara wa Julai ambao tayari waliufanyia kazi lakini pia walipwe mafao
yao maana waliitumikia Serikali kwa uadilifu na vyeti vyao hivyo vya
elimu ya msingi.

Comments
Post a Comment