Spika wa Bunge, Job Ndugai, ameikubali barua
aliyoandikiwa na Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekti wa CUF
anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kuwatimua uanachama
wabunge wake wanane wa viti maalum.
Hatua hiyo ya Spika Ndugai inamaanisha kuwa wabunge
hao wamepoteza viti vyao Bungeni na chama hichi kitatakiwa kuwateua
wanachama wengine kuziba nafasi hizo.
Taarifa iliyotolewa na Bunge jioni hii inasema Spika amechukua uamuzi huo kwa mujibu wa ibara ya 67(1)(b).
Spika ametoa uamuzi huo siku moja tu baada ya kueleza
kupokea barua ya Profesa Lipumba na kusema anaitafakari kabla ya kutoa
uamuzi wake.
Taarifa ya Bunge imewataja wabunge waliopoteza nafasi
zao kuwa ni Severina Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mwassa na Riziki
Mngwali.
Wengine ni Raisa Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Al-Qassmy na Halima Mohammed.
Profesa Lipumba alisema wiki iliyopita kuwa wanachama hao wamefukuzwa kutokana na utovu wa nidhamu na kukiuka katiba ya chama.
Alisema wabunge hao waliitwa ili kujitetea lakini
wakakaidi na hivyo Baraza Kuu la Uongozi halikuwa na uamuzi mwingine
zaidi ya kuwafukuza uanachama.
Pamoja nao, wabunge wengine wawili nao waliitwa lakini
wamesalimika kwa sababu waliitaarifu kamati hiyo kuwa wamebanwa na
majukumu mengine.
Aidha, Profesa Lipumba alisema timuatimua hiyo
itaendelea ikimhusisha pia Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharif
Hamad, ambaye hajafika makao makuu ya chama hicho kwa kipindi kirefu.

Comments
Post a Comment