NAMUONA MAGUFULI

 

Nayaona mambo leo, naona maendeleo
Naona upendo leo, bila ya kuwa na cheo
Naona kwa macho leo, bila tv na video 
Na kila nikitazama, namuona magufuli 

Nimeiona dhamira, imeelekea dira
Imenijia twasira, kwa jamii na hadhira.
Tulilala tirarira, tumefunguliwa nira
Na kila nikitazama, namuona magufuli

Nimeiona jamii, ikipata matibabu
Nimeona watalii, wa nchi za ughaibu 
Kelele sizisikii, tunasonga taratibu 
Na kila nikitazama, namuona magufuli

Nimeona mafisadi,wakipata tabu sana
Muda umetaradadi,wamebanwa mbavu sana 
Kulitimiza kusudi,yataka moyo mpana 
Na kila nikitazama, namuona magufuli 

Nimeona barabara,zikijengwa kila leo 
Miundo mbinu imara,madaraja mshangao 
Maendeleo mawio,maendeleo machweo 
Na kila nikitazama, namuona magufuli 

Nawaona wakulima,wakifurahi sokoni 
Nawaona kina mama,na tabasamu usoni 
Majizi wenye lawama,na miguno chinichini 
Na kila nikitazama, namuona magufuli 

Nimesikia mapato, na kodi vimeshibana 
Nimesikia vipato halali vinapishana 
Nimesikia vidato na kazi vinaendana 
Na kila nikitazama, namuona magufuli 

Nimelisikia neno, nchi yetu ni tajiri 
Tuna makucha na meno,kiuchumi kunawiri
Tuna kalamu na wino,kuandika histori 
Na kila nikitazama, namuona magufuli 

Nimeyaona madege, bombadia na boeing 
Ya kufika kila pande, ya nchi na ugenini 
Na makabwela tupande, tufike ughaibuni 
Na kila nikitazama, namuona magufuli 

Basi nakuomba mungu umpe makazi mema 
umtangulie mungu, katufikisha salama 
Hata nasi wa mafungu, tunaiona neema 
Na kila nikitazama, namuona magufuli

Comments

  1. Na kila iitwayo leo, namkumbuka Magufuli

    ReplyDelete

Post a Comment